Header Ads

RAIS MAGUFULI AZUIA KUBOMOLEWA KWA NYUMBA 1, 900 MWANZA


Rais John Magufuli amezuia kuondolewa kaya zaidi 1,900 zinazoishi katika nyumba zilizopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Mwanza hadi itakapofanyika tathmini kwa sababu wananchi hao ni wapigakura wake.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Februari 24, 2018 baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Mwanza  ambapo walimweleza kuwa uwepo wa kaya hizo unakwamisha ujenzi wa uwanja huo.
Akijibu jambo hilo, Rais Magufuli amesema wasiondolewe hadi pale watakapolipwa madai yao huku pia akiwataka wananchi hao kutoendeleza makazi yao.
"Hawa watu ndio walionipa kura, pamoja na hivyo msiwaondoe hadi pale mtakapokamilisha kuwalipa madai yao," amesema Rais Magufuli.
Ikumbukwe kuwa Oktoba mwaka jana, Rais Magufuli aliagiza kusitishwa kwa ubomoaji wa nyumba za wananchi zaidi ya 2,000 wanaodaiwa kuvamia eneo la uwanja huo, kituo cha polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa daraja la juu la waenda kwa miguu eneo la Furahisha jijini Mwanza.
Rais Magufuli aliagiza ubomoaji huo usitishwe hadi atakapotolea uamuzi suala hilo.
Meneja wa uwanja huo, Ester Mandale alimweleza Rais Magufuli kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa jengo la wasafiri, uwanja kukosa uzio pamoja na ndege kuzuiwa kubeba samaki.
Amesema baada ya ndege kuzuiwa kusafirisha samaki kwenda nchi za nje, wanalazimika kusafirisha kwa kutumia magari wakati wenzao wa Kenya wanatumia ndege, hivyo kuikosesha Serikali mapato.Akizungumzia changamoto hiyo, Rais Magufuli alimwagiza meneja huyo kufanya tathmini inayohitajika katika ujenzi wa jengo la usafiri pamoja na uzio kisha aiwasilishe kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.Kuhusu usafirishaji wa samaki, Rais Magufuli aliagiza kufanya uchunguzi kwa wenzao wa Kenya kujua wanasafirishia kwa gharama kiasi gani.
Rais Magufuli ameondoka jijini Mwanza na kuelekea Chato kwa ajili ya mapumziko mafupi kabla ya kuelekea Ikulu jijini Dar es Salaam.

No comments