Tuzo Komla Dumor 2018: BBC yaanza kumtafuta mwandishi mwingine nyota Afrika
Shirika la utangazaji la Uingereza BBC limeanza tena mchakato wa kumtafuta nyota mpya wa uandishi kuhusu Afrika ambaye atatunukiwa Tuzo ya BBC ya Komla Dumor mwaka huu.
Huu utakuwa mwaka wa nne kwa tuzo hiyo kutolewa.
Wanahabari kutoka kote barani Afrika wanaombwa kuwasilisha maombi ya kushindania tuzo hii, ambayo hulenga kufichua na kuendeleza waandishi wapya wenye vipaji kutoka Afrika.
Mshindi atafanya kazi katika makao makuu ya BBC London kwa miezi mitatu, ambapo atajipatia ujuzi zaidi na uzoefu.
Siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ni 23 Machi 2018 saa 23:59 GMT.
Tuzo hiyo ilianzishwa kwa heshima ya Komla Dumor, mtangazaji wa BBC mwenye kipaji cha kipekee kutoka Ghana aliyefariki ghafla akiwa na miaka 41 mwaka 2014.
Tuzo ya mwaka huu itazinduliwa katika makao makuu ya Ghana, Accra
Tuzo hiyo itatolewa kwa mwandishi wa kipekee anayeishi na kufanya kazi Afrika, ambaye anaunganisha ujuzi wa kipekee kuhusu uanahabari, ustadi katika utangazaji, na kipaji katika kusimulia taarifa kuhusu Afrika na ambaye ana ndoto na uwezo wa kuwa nyota wa uandishi siku za usoni.
Pamoja na kufanya kazi makao makuu ya BBC London, mshindi pia atasafiri Afrika na kuangazia taarifa moja - ambayo itaenezwa kote barani na duniani
Washindi wa awali ni Nancy Kacungira kutoka Uganda, Didi Akinyelure kutoka Nigeria na Amina Yuguda, pia kutoka Nigeria Nigeria.
Kwa taarifa yake kuu, Amina aliangazia hatari inayolikabili Ziwa Victoria nchini Uganda, ziwa kubwa zaidi la maji yasiyo na chumvi Afrika, ambalo wanasayansi wanaonya kwamba linakabiliwa na hatari ya 'kufariki'.
"Kuwa mshindi wa Tuzo ya BBC ya Komla Dumor mwaka 2017 kulikuwa kama mwanzo mpya kwa taaluma yangu. Kupata jukwaa la kimataifa, na kutambuliwa katika ngazi ya kimataifa, ni kama nilikuwa nimefika," Amina alisema.
"Wakati wa kipindi changu BBC, nilifahamu umuhimu wa ukweli, kuangazia pande zote kwenye taarifa na kutopendelea upande wowote, na pia nilijifunza mengi kuhusu jinsi ya kuzifanya taarifa za Afrika zivutie kimataifa.
"Tunajivunia jinsi Komla alipoiwasilisha Afrika kwa ulimwengu, na ni heshima kubwa kwangu kuendeleza kazi hiyo."
Amina atashiriki katika hafla ya uzinduzi wa tuzo ya 2018, pamoja na Jamie Angus, mkurugenzi katika BBC World Service.
Akiongea kabla ya uzinduzi, alisema:
"Ni heshima kuwa hapa Ghana, nyumbani kwa Komla, kuwa pamoja na familia yake na marafiki zake, kusherehekea kazi yake na kumtafuta mwandishi atakayekuwa nyota wa uandishi Afrika siku za usoni.
"Washindi watatu wa awali - Nancy, Didi na Amina - wote wamedhihirisha kwamba ni waandishi wenye kipaji, wenye ufahamu wa ndani kuhusu bara hili, na wenye ujuzi kuhusu jinsi ya kuwasiliana na wasikilizaji na watazamaji Afrika.
"Tunasubiri kwa hamu kumpata mwandishi mwingine wa kipekee kutoka bara hili na kumkaribisha kama mshindi wa Tuzo ya BBC ya Komla Dumor."
No comments